Kazi ya Ujenzi wa Kiwanda cha Kusafisha Chumvi Nangurukuru – Kilwa Yaendelea
Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, ameweka wazi kuwa Serikali inaendelea kuimarisha thamani ya madini ya Tanzanite baada ya kufanya marekebisho muhimu ya Kanuni za Eneo Tengefu la Mirerani za Mwaka 2019. Marekebisho haya yanaruhusu biashara ya madini hayo kufanyika katika masoko mengine ya ndani na nje ya Mirerani kwa utaratibu maalum, ikiwemo masoko makubwa ya madini kama Arusha, Mwanza, Mbeya, Dar es Salaam, na Zanzibar.
Dk. Kiruswa ameyasema hayo wakati wa kikao cha Bunge, ambapo alijibu swali la Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe. Mrisho Gambo, aliyehoji kuhusu lini Serikali itaruhusu uuzaji wa madini ya Tanzanite katika masoko ya ndani.
Kwenye majibu yake, Dk. Kiruswa alibainisha umuhimu wa biashara ya Tanzanite, na kusema kuwa mwaka 2024, Wizara ya Madini iliweka utaratibu mpya wa biashara ya madini hayo kupitia Kituo cha Uuzaji wa Pamoja wa Tanzanite (Tanzanite Exchange Centre – TEC). Utaratibu huo utaruhusu biashara ya Tanzanite ghafi nje ya Mirerani, kwa yeyote mwenye leseni kubwa ya ukataji madini. Aidha, biashara ya Tanzanite iliyokatwa na kung’arishwa itaruhusiwa kufanyika endapo mhusika atakuwa na leseni yoyote ya biashara au ukataji wa madini.
Katika mwaka wa fedha 2024/25, Wizara pia imepanga kufanya minada na maonesho ya madini ya vito ikiwemo Tanzanite katika maeneo ya Arusha, Mirerani, Mahenge, Dar es Salaam, na Zanzibar. Minada ya kwanza ilifanyika Desemba 14, 2024, katika eneo la Mirerani, mkoani Manyara.
Kuhusiana na ujenzi wa Kiwanda cha Kusafisha Chumvi, Dk. Kiruswa ametangaza kuwa Serikali inaendelea na hatua za ujenzi wa Kiwanda hicho katika eneo la Lingaula, Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi. Huu ni mpango wa kutatua changamoto zinazowakabili wazalishaji wa chumvi, hasa katika mikoa ya kusini.
Akiwa anajibu swali la Mbunge wa Kilwa Kusini, Mhe. Ally Mohamed Kassinge, kuhusu maendeleo ya kiwanda hicho, Dk. Kiruswa alifafanua kuwa eneo la mradi umepimwa, hati ya umiliki imepatiwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), na mtambo wa kusafisha chumvi umenunuliwa. Awamu ya kwanza ya mtambo umefika nchini, na taratibu za usafirishaji zinaendelea. Ujenzi wa jengo kwa ajili ya mtambo umeanza na unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 2025.
Hatua hizi zinaimarisha juhudi za Serikali kuboresha sekta ya madini na kuongeza thamani ya rasilimali za taifa, huku zikilenga kukuza biashara ya Tanzanite na kuongeza uzalishaji wa chumvi nchini.