Dar es Salaam. Maabara ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imepata cheti cha kimataifa cha ubora wa huduma za maabara. Cheti cha ISO 15189:2012 kilitolewa mwezi Oktoba 2024 na Shirika la Viwango vya Ubora wa Maabara kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADCAS).
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Mpoki Ulisubisya, alitangaza kupata cheti hicho leo, Desemba 30, 2024, akisisitiza umuhimu wa ubora wa vipimo kwa wagonjwa na taifa kwa ujumla. Dk Ulisubisya alieleza kuwa cheti hicho kitachochea utalii wa matibabu, kuchangia ukuaji wa uchumi, kuongeza mapato ya Serikali, na kuunda ajira kwa Watanzania.
Alifafanua kuwa MOI imejikita kama kituo cha matibabu kinachotambulika barani Afrika, kikivutia wagonjwa kutoka nchi jirani na sehemu nyingineza duniani kutibiwa Tanzania. "Kupata ithibati ya ubora ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazotimiza viwango vya kimataifa bila haja ya kusafiri nje ya nchi," alisema.
Dk Ulisubisya alisisitiza kuwa majibu ya vipimo vya maabara yanayotolewa na MOI yamehakikishwa kuwa na ubora wa juu, na usahihi wa kimataifa, hali inayoongeza imani kwa wagonjwa ndani na nje ya Tanzania. Aidha, aliongeza kuwa huduma za kimataifa zitasaidia Watanzania kuokoa gharama za matibabu nje ya nchi, huku zikiongeza mapato ya Serikali kupitia wageni wanaokuja kwa matibabu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maabara, Nsiande Ndoso, alisema taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 1996 bila ithibati ya ubora, na kuanza mchakato wa kutafuta uthibitisho huo mwaka 2021, ambao umesaidia kupata hati hiyo baada ya kutimiza vigezo vilivyotakiwa. Alisisitiza kuwa maabara ina uthibitisho wa kimataifa katika utendaji wa kufanya uchunguzi mbalimbali, na vipimo vinavyofanyika nchini vinalingana na viwango vya kimataifa.