Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imeanzisha vipaumbele vyake kwa mwaka 2025, ikijumuisha ujenzi wa miundombinu ya shule, nyumba za walimu, mabwalo, majiko, matundu ya vyoo, maktaba, maabara za sayansi, na ofisi za walimu.
Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dk. Erasmus Kipesha, akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, alisisitiza kuwa TEA itaendelea kuboresha mazingira ya kujifunza, pamoja na upatikanaji wa vitabu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, na vifaa maalum kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Katika juhudi za kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika sayansi na teknolojia, Kipesha alitangaza mpango maalum wa kuwasaidia wanafunzi wa kike kujiunga na michepuo ya sayansi katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.
Vipaumbele vingine vya TEA vinajumuisha ujenzi na ukarabati wa majengo ya vyuo vya elimu ya juu, upanuzi wa kumbi za mihadhara, na miradi mingine ya kuongeza fursa za elimu nchini.