Dodoma. Chama cha NCCR-Mageuzi kimefanya uchaguzi wake wa viongozi ambapo Haji Khamis amechaguliwa kuwa mwenyekiti, akichukua nafasi ya James Mbatia. Katika uchaguzi huo, Khamis alikamata kura 508 kati ya 511, huku kura moja ikimpinga na mbili zikiharibika.
Khamis, ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, amekuwa akikabiliwa na jukumu la kuendeleza chama baada ya kuondolewa kwa Mbatia.
Mkutano Mkuu wa NCCR-Mageuzi ulifanyika leo Jumamosi Machi 29, 2025, jijini Dodoma, ukiwa na agenda ya uchaguzi wa viongozi wa kitaifa na wa ngazi nyingine.
Katika uchaguzi huo, Joseph Selasini alifanikiwa kutetea nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Tanzania (Bara) kwa kupata kura 483, huku kura 12 zikiharibika na 16 zikimkataa. Selasini amekuwa akiongoza mageuzi ya uongozi ndani ya chama hicho cha upinzani.
Kwa upande wa Zanzibar, nafasi ya Makamu wa Tanzania Zanzibar imechukuliwa na Laila Rajabu Khamisi, ambaye alipata kura 478, huku kura 15 zikimkataa na 18 zikiharibika.
Wajumbe walikabiliwa na uchaguzi wa nafasi nyingi, ambapo wengi walipiga kura za ndiyo na hapana kutokana na kuwa na wagombea mmoja mmoja kwa nafasi hizo.