Kampuni ya Ujenzi na Mawasiliano ya China (CCCC) tawi la Tanzania imekiri kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari ili kufanikisha utekelezwaji wa shughuli zake zinazolenga maendeleo ya taifa.
Kiongozi wa CCCC Tawi la Tanzania, Li Yuliang, amesema kuwa kampuni hiyo imepata mafanikio makubwa kupitia shughuli zake na kupongeza vyombo vya habari kwa wajibu wake katika kuhabarisha umma kuhusu matukio ya kampuni hiyo.
Majadiliano yaliyohusisha waandishi wa habari na wahariri yalilenga kutathmini shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo, pamoja na kujadili changamoto na kutoa mapendekezo ya kuboresha utendaji zaidi.
“Ni matumaini yangu kuwa mwaka 2025 tutaimarisha ushirikiano, kujenga uhusiano mzuri na kufanya kazi kwa viwango vya juu zaidi,” alisema Yuliang.
Kampuni hiyo ilieleza malengo yake, mafanikio na michango yake ya kijamii kwa mwaka 2024 katika mkutano huo.
Kampuni hiyo inatekeleza miradi mbalimbali katika maeneo kama Masasi, Mtwara, Arusha, na Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).
Pamoja na shughuli za ujenzi, kampuni hiyo pia inahamasisha jamii kujifunza lugha ya Kichina kwa kutembelea shule na vyuo, kuzungumza na wanafunzi, na kugawa vitabu.
Aidha, CCCC imeshiriki katika kutembelea makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu, watoto yatima na kutoa misaada ya kibinadamu.