Khartoum, Sudan
Jeshi la Sudan limefanya hatua kubwa kwa kukomboa mji wa Wad Madani, ambao ni mji muhimu mashariki mwa nchi, kutoka kwa vikosi vya wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF). Huu ni mabadiliko makubwa katika vita vinavyoendelea kwa karibu miaka miwili kati ya upande hizi mbili.
Picha zinazoonekana kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha raia wakifurahia ushindi huo, huku wanajeshi wakijumuika na umma katika mji huo, ambao uko kilomita 140 kusini mwa mji mkuu, Khartoum.
Kiongozi wa RSF, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, amekiri kupitia ujumbe wa sauti kwamba vikosi vyake vimelazimika kukabiliana na mashambulizi makali ya angani yaliyotolewa na ndege zisizo na rubani zinazodaiwa kutengenezwa na Iran.
Licha ya kupoteza mji, Hemedti ameahidi kuendelea na mapambano, akionya kwamba vita vinaweza kudumu kwa zaidi ya miaka 20, lakini hawezi kuacha hadi ushindi upatikane.
Wad Madani ni mji wa kimkakati, ukiwa ni kiungo muhimu cha usafirishaji na shughuli za kiuchumi kati ya Khartoum na maeneo ya kusini mwa Sudan. Mafanikio haya ya jeshi yanaweza kubadilisha mwelekeo wa vita hivi vya muda mrefu.