Njombe. Wananchi wa Ludewa, mkoani Njombe, wameipongeza Serikali kwa hatua zake za kuboresha huduma za matibabu, hususan baada ya kukabidhiwa vyombo vya usafiri vikiwemo pikipiki mbili na gari moja la kubebea wagonjwa.
Katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika leo, Desemba 29, 2024, wananchi wamesema msaada huu utawasaidia katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa usafiri wa haraka, hususan kwa wanawake wajawazito na wagonjwa wengine wanaohitaji matibabu ya dharura.
Mary Mlelwa, mmoja wa wakazi wa Ludewa, alieleza jinsi gari hilo litakavyosaidia kuwafikisha wagonjwa hospitalini haraka, hivyo kupunguza vifo visivyo vya lazima. "Gari hii itatusaidia sana, hasa kwa kinamama wajawazito," alisema Mlelwa.
Dk. Isack Chussi, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ludewa, alibainisha umuhimu wa usafiri wa vyombo vya moto kutokana na jiografia ya wilaya hiyo. Alisema kuna vituo 81 vya afya ambavyo vinahitaji usafiri, ili wagonjwa wawahi matibabu wanapokumbana na dharura.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Godlove Katemba, aliongeza kuwa wilaya hiyo ina upungufu wa watumishi wa afya, ambapo wanaohitajika ni 1400 lakini wanapatikana 450 pekee.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Castory Kibasa, alisema vyombo hivyo vimetolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ili kusaidia katika kusafirisha wagonjwa kutoka eneo moja la huduma hadi lingine.
Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamonga, aliahidi kuendelea kushirikiana na wananchi katika juhudi za kuboresha maendeleo ya wilaya. "Nilijitahidi kutafuta magari kutoka maeneo mbalimbali, na nitendelea kuwasaidia," alisema Kamonga.