Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatarajia kuanza utoaji wa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 15 kwa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, huku benki ya CRDB ikichukua jukumu la usimamizi wa mikopo hiyo.
Benki hiyo ilitangazwa rasmi katika mkutano maalumu wa utambulisho wa mikopo, ambapo Mkurugenzi wa CRDB Foundation, Tully Mwambapa, alieleza kuwa wataunganisha jamii kwa kutoa elimu kuhusu upatikanaji wa mikopo ya asilimia 10 na umuhimu wa kurejesha fedha hizo kwa wakati.
“Tunakusudia kuwafaidi wanawake, vijana, na wajasiriamali kutoka katika makundi maalumu ili waweze kuboresha maisha yao kupitia programu ya Serikali na mpango wetu wa Imbeju,” alisema Mwambapa.
Kwa kuzingatia uhitaji mkubwa juu ya mikopo katika jamii, CRDB ilianzisha kampuni yake tanzu ya Crdb Bank Foundation mwaka 2023, yenye lengo la kukuza ujumuishi wa kifedha na kiuchumi.
“Programu ya Imbeju inawafikia wanawake, vijana, na makundi maalumu katika sekta mbalimbali za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na biashara, kilimo, na teknolojia. Tunatarajia kuhakikisha kwamba huduma zetu zinawafikia walengwa wote nchini,” alifafanua Mwambapa.
Hadi mwezi Januari 2025, CRDB Bank Foundation inatarajiwa kutoa elimu ya fedha na mafunzo kwa wapataji zaidi ya 800,000, huku jumla ya mitaji ya Sh bilioni 20.2 ikitekelezwa, ikiwa ni pamoja na zaidi ya Sh bilioni 14.1 kwa wakazi wa Dar es Salaam.
CRDB pia imekabidhi vitendea kazi vyenye thamani ya Sh milioni 45 kwa maafisa wa maendeleo ya jamii ili kuimarisha ufanisi wa kazi zao, pamoja na kompyuta 21 kwa ajili ya kusimamia mikopo hiyo kwa ufanisi.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, hadi mwaka 2024, benki hiyo itakuwa imetoa mikopo ya Sh trilioni 10.4, ambapo asilimia 30 ya mikopo hiyo zitatolewa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alitoa taarifa kuwa zaidi ya wananchi 945 wameshaomba mikopo hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kufuata maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu upatikanaji wa mikopo kwa kila Mtanzania mwenye sifa.
“Ni wajibu wetu kusimamia na kutenda haki katika utoaji wa mikopo hizi, kuhakikisha kwamba dhamira ya Rais inatekelezwa ipasavyo na watu wanapata matokeo chanya baada ya kutumia mikopo,” alisema Mpogolo.
Hii ni hatua kubwa katika kuimarisha maendeleo ya kifedha miongoni mwa jamii ya Dar es Salaam na ni ishara ya kuzingatia kazi zinazofanywa na benki hiyo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.