Benki ya Akiba imezindua kampeni mpya ya kidijitali ijulikanayo kama ‘Twende Kidijitali’ katika juhudi za kutoa suluhisho la changamoto za kifedha kwa wateja.
Kampeni hii, iliyozinduliwa mwanzoni mwa mwezi Desemba 2024, inakusudia kuboresha uzoefu wa wateja kupitia huduma za kifedha za kisasa, haraka, na za kuaminika.
Kampeni hiyo inahamasisha matumizi ya huduma za kidijitali kama vile ACB Mobile, Internet Banking, VISA, na Akiba Wakala.
Katika uzinduzi wa kampeni, Dk. Danford Muyango, Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa ACB, alisisitiza umuhimu wa teknolojia ya kisasa katika kuboresha huduma kwa wateja.
Dk. Muyango aliongeza kuwa kampeni hiyo inafanyika sambamba na kampeni nyingine ya msimu wa sikukuu, ‘Twende Kidijitali, Tukuvushe Januari’, inayolenga kusaidia wateja katika kipindi ambacho mara nyingi kinakuwa kigumu kifedha.
“Kampeni hii ni mwendelezo wa lengo la Benki ya Akiba kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali na kuhamasisha wateja kufaidi teknolojia katika kutatua changamoto zao za kifedha,” alisema Dk. Muyango.
Wateja wanaweza kushiriki katika kampeni kwa kufanya miamala ya kidijitali ambapo watapimwa kulingana na idadi na thamani ya miamala yao. Wateja walio na ushiriki mkubwa watapata nafasi ya kushinda zawadi za fedha taslimu.
Vigezo vingine vya kushiriki ni pamoja na kutoa maoni kuhusu huduma za kidijitali, ambapo washiriki wataweza kushinda katika droo ndogo. Aidha, wateja wanaowaalika wengine kufanya miamala kwa njia ya ATM, POS, Wakala, Mobile Banking, au Internet Banking watajishindia zawadi.
“Benki ya Akiba inakaribisha wateja wote kujiunga nasi katika safari hii ya kidijitali kwa kutembelea matawi yetu au kuangalia huduma zetu za kidijitali,” alisisitiza.