Wananchi wa Arusha wanasherehekea bidhaa mbalimbali za Nishati Safi ya Kupikia zinazotolewa na Serikali katika maonesho yanayoendelea, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Wakizungumza siku ya Machi 6, 2025, baada ya kutembelea Banda la REA na kujionea teknolojia za majiko ya Nishati Safi ya Kupikia, wananchi hao walionyesha kuridhishwa na bidhaa hizo, wakisema zinafaida kubwa katika kulinda mazingira na kurahisisha mchakato wa kupika.
Ester Mwasigo, mkazi wa Dodoma, alieleza furaha yake kuhusu majiko yaliyozinduliwa, akisema, “Teknolojia iliyotumika ni nzuri na majiko haya tunayapenda.” Alitoa wito kwa wananchi kujifunza kutoka kwenye banda la REA ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mwasigo aliongeza, “Tunatumia gharama kubwa kununua mkaa wa kawaida; mimi ni balozi wa teknolojia hii. Serikali imefanya jambo muhimu na inahitajika kutoa elimu zaidi kwa wananchi.”
Mwajuma Tarek, mkazi wa Muriet Jijini Arusha, alisisitiza umuhimu wa kampeni zinazofanywa na Serikali za kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi, akiongeza kuwa kila mwanamke amehamasika kwenye mchakato huu wa mabadiliko.