Mamlaka za Korea Kusini zimedai kuwa watu 179 wamefariki dunia katika ajali ya ndege ya Shirika la Jeju, iliyokuwa imebeba jumla ya abiria na wahudumu 181, ambapo abiria wawili pekee ndio waliweza kuokolewa wakiwa hai.
Ndege hiyo aina ya Boeing 737-800 ilipata ajali saa 6:03 usiku wa kuamkia leo, Desemba 29, 2024, katika Uwanja wa Kimataifa wa Muan nchini Korea Kusini, muda mfupi baada ya kukosa kutua kwa kutumia tairi zake.
Picha na video zilizovuja zinaonyesha ndege hiyo ikitua kwa kasi kwa kutumia sehemu ya mwili wake, jambo lililosababisha kulipuka na kusababisha madhara makubwa.
Ndege hiyo ilikuwa ikitokea Bangkok, Thailand kuelekea Korea Kusini, ambapo abiria wawili waliokuwemo ni raia wa Thailand, lakini waliofariki ni raia wa Korea Kusini.
Hadi kufikia saa 3:30 asubuhi, mabaki ya miili 120 ya abiria waliokuwemo ndani ya ndege hiyo yalikuwa yamepatikana, huku juhudi za maofisa wa Mamlaka ya Kupambana na Majanga ya Moto zikiendelea kutafuta miili iliyosalia.
Majeruhi wawili waliokolewa, mmoja akiwa abiria na mwingine mhudumu, wamepelekwa hospitali iliyoko karibu na uwanja wa ndege. Taarifa zinaeleza kuwa Kaimu Rais wa Korea Kusini, Choi Sang-mok, ameendelea kufuatilia maendeleo ya ajali hiyo eneo la tukio.