Babati: Mkaazi wa Mtaa wa Sawe, Kata ya Maisaka, mjini Babati, amefariki dunia katika tukio ambalo linaaminika kuwa linahusishwa na ulaji wa pombe nyingi za kienyeji.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani, alithibitisha kifo hicho katika mkutano wa waandishi wa habari leo, Januari 8, 2025, na kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusiana na kifo hicho.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Sawe, John Paul, alieleza kwamba Yona Angres alifariki baada ya kunywa pombe nyingi za kienyeji. "Watu walio karibu naye wamesema kuwa Angres alikunywa pombe nyingi za kienyeji kabla ya kifo chake," alisema Paul.
Mkazi wa eneo hilo, Isack Dere, aliwakumbusha wanajamii kufuata sheria za afya na kunywa pombe zilizothibitishwa. "Kuna kiwanda kizuri cha vinywaji Babati, kwa nini mtu akose kujijali na kutumia pombe za kienyeji zisizojulikana?" aliongeza Dere.
Asia Juma, mkazi mwingine, alieleza kuwa Angres alikuwa akifanya vibarua kama kubeba maji. "Nadhani alikosa chakula siku hiyo, na hiyo inaweza kuwa sababu ya kifo chake baada ya kunywa pombe nyingi za kienyeji," alisema Juma.