Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Kupitia juhudi za kuboresha viwango vya ubora wa bidhaa, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetangaza kupata ithibati ya kimataifa kwa maabara zake 12. Hii inahakikisha kwamba matokeo ya sampuli zinazopimwa yanakuwa na uaminifu ndani na nje ya nchi.
Hayo yameelezwa leo Machi 18, 2025, na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Ashura Katunzi, wakati wa mazungumzo na waandishi wa habari kuelekea miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Kupitia maabara zetu za kisasa, tumepima sampuli zaidi ya 118,059 na kufanyia ugezi vifaa 36,808. Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa sokoni zinakidhi viwango vya ubora,” alisema Dk. Katunzi.
Amesema kuwa TBS imewekeza katika teknolojia mpya, ikiwemo mashine ya kupima shinikizo la maji, ambayo inaweza kupima mabomba ya maji yenye kipenyo kuanzia milimita 12 hadi milimita 800 (inchi 0.5 hadi 32).
Dk. Katunzi pia ameonya kuhusu matumizi yasiyofaa ya vilevi, akisisitiza kuwa tatizo haliko katika ubora wa bidhaa hizo, bali ni matumizi yasiyo sahihi.
“Tatizo sio kwamba vilevi vilivyoko sokoni havina ubora, bali ni matumizi yasiyo sahihi. Watu wanakunywa kwa kiwango kisichofaa na bila kuchanganya kama inavyotakiwa. Vijana, tukizidisha matumizi mabaya ya vilevi, tunahatarisha nguvu kazi ya taifa kwa siku zijazo,” aliongeza.
Ametoa wito kwa jamii kuendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vilevi ili kuhakikisha afya na ustawi wa vijana na jamii kwa ujumla.