Na Mwandishi Wetu,
KAMATI Tendaji ya Usimamizi wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) imeeleza kuridhishwa na utoaji wa huduma za mradi huo katika Halmashauri za Wilaya ya Mbarali na Mbeya Vijijini Mkoani Mbeya.
Hayo yamebainishwa leo Jumapili (Machi 16, 2025) Mkoani Mbeya wakati wa ziara ya wajumbe wa kamati hiyo kukagua shughuli za utekelezaji wa mradi ikiwa ni juhudi zinazofanywa na Serikali kuhamasisha kuhusu uhifadhi wa mazingira na urejeshwaji wa uoto wa asili nchini.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa kamati, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Maji amesema kamati hiyo imeridhishwa na ushirikiano na juhudi zinazofanywa na Serikali kupitia mradi huu katika kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kama njia muhimu za kuboresha ustawi wa maisha.
“Tumejionea miradi ya utunzaji wa vyanzo vya maji, upandaji miti, pamoja na miradi ya kuboresha maisha ya jamii kama ufugaji, uchimbaji wa visima na ufugaji wa nyuki. Miradi hii inalenga kusaidia jamii na tumeona mwitikio chanya kutoka kwa wanajamii,” amesema Mkurugenzi Msaidizi.
Aidha, aliongeza kuwa hatua zilizochukuliwa na mradi katika kuweka miradi ya kijamii na kiuchumi zimejenga mwamko miongoni mwa wananchi na kuwapa motisha katika kutunza mazingira, ikiwemo kupanda miti na kuhifadhi uoto wa asili.
Mafanikio ya mradi huu yatasaidia jamii ya Mbarali na Mbeya Vijijini kuwa sehemu muhimu ya kuchagiza ajenda ya uhifadhi wa mazingira kupitia fursa za miradi zinazoibuliwa na jamii, na kuboresha ukuaji wa kipato katika ngazi ya kaya.
“Wananchi wamehamasika kupitia miradi hii…. tumeshuhudia uchimbaji wa visima na ujenzi wa majosho kwa ajili ya mifugo, shughuli hizi ni msingi mkuu wa maisha ya kiuchumi kwa wananchi wa vijijini. Tunasisitiza umuhimu wa miradi hii kuendelea kutunzwa ili inufaishe vizazi vya sasa na vijavyo,” alisisitiza Mkurugenzi Msaidizi.
Alipongeza Serikali kwa kuziunganisha Wizara katika kuunda kamati ya kitaifa ya usimamizi wa mradi huu, na kuahidi kuwa Wizara ya Maji itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha malengo ya mradi yanatimia katika kuimarisha hifadhi endelevu ya mazingira na urejeshwaji wa uoto wa asili.
Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Makamu wa Rais alisema kupitia mradi huo Ofisi hiyo itaendelea kujenga uwezo kwa makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwa ni pamoja na wanawake na vijana, ili waweze kuendesha shughuli endelevu za uhifadhi wa mazingira na kujiongezea kipato.
“Ziara hii imeweza kutoa picha halisi ya hali ya uhifadhi wa mazingira katika jamii za Mbarali na Mbeya Vijijini, sasa tunaona jinsi wanavyoweza kunufaika kupitia fursa mbalimbali, ikiwemo uvunaji wa asali ambao umewawezesha kuongeza kipato,” alisema.
Kamati hiyo ya kitaifa ya Mradi wa SLR ilitembelea jumla ya miradi nane ya uhifadhi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na mradi wa chanzo cha maji, bustani ya miche, josho la mifugo, mradi wa maji, banio la mifugo, na uhifadhi wa misitu.
Mkakati wa SLR umewekwa kwa ajili ya kusaidia uhifadhi wa mazingira na umepewa fedha za ujazo wa shilingi bilioni 25.8 kwa ajili ya utekelezaji wake. Mradi huu ulianza mwaka 2021 na unatarajia kukamilika mwaka 2025, ukiwanufaisha wananchi katika Mikoa 5, Halmashauri 7, Kata 18 na vijiji 54.