Marekani. Utajiri wa Elon Musk, tajiri namba moja duniani, umeendelea kushuka kwa dola bilioni 22.2 (Sh57 trilioni) ndani ya siku moja.
Katika Desemba 2024, utajiri wake ulifikia kilele cha Dola 480 bilioni, lakini sasa umepungua kwa takriban dola bilioni 116 hadi kufikia dola bilioni 364.3 Februari 2025, kulingana na taarifa kutoka kwa jarida la Wealth.
Kuporomoka huku kunahusishwa moja kwa moja na kupungua kwa thamani ya hisa za kampuni yake kubwa, Tesla, ambapo hisa zake zimepungua kwa asilimia 30 tangu Desemba 2024.
Hisa hizo zimeendelea kudorora zaidi kwa asilimia 21 tangu Januari 2025, hali ambayo imesababisha msukosuko mkubwa kwa wawekezaji na kupunguza thamani ya soko la bidhaa za kampuni hiyo.
Tesla, ambayo inachangia zaidi ya nusu ya utajiri wa Musk, imekumbwa na changamoto kadhaa mwaka huu. Mauzo ya Tesla yamekumbwa na kushuka kwa kiwango kikubwa katika masoko muhimu, hasa barani Ulaya, ambapo mauzo yalishuka kwa asilimia 50 Januari 2025.
Hali hii imefanya jumla ya hisa za kampuni kushuka chini ya Dola 1 trilioni kwa mara ya kwanza tangu Novemba 2024.
Aidha, ushindani mkali kutoka kwa kampuni za magari ya umeme kama BYD ya China umeongeza shinikizo kwa Tesla, huku kampuni hiyo ikivutia wateja kwa bei nafuu na teknolojia ya kisasa.
Pia, siasa za Elon Musk zimeonekana kuathiri Tesla, kwani nafasi yake katika utawala wa Trump imepunguza imani ya wawekezaji. Wengi wanahisi kuwa shughuli zake za kisiasa zinachangia kupunguza muda wake wa kuongoza kampuni.
Mabadiliko ya sera, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa ruzuku za magari ya umeme na kulegezwa kwa sheria za uchafuzi wa mazingira, yanaweza kuathiri mapato ya Tesla kwa kiasi kikubwa.
Mahitaji ya magari ya umeme yamepungua huku ushindani ukiongezeka. Makampuni kama BYD na Volkswagen yanaendelea kutoa magari ya bei nafuu na teknolojia ya kisasa, hali inayosababisha shinikizo zaidi kwa Tesla.
Pamoja na changamoto hizi, Musk anatarajia kuanzisha majaribio ya teksi zinazojiendesha (robotaxi) jijini Austin, Texas, ifikapo Juni 2025. Hata hivyo, wawekezaji wanaendelea kuwa na mashaka kuhusu uwezo wa Tesla kushindana na makampuni mengine yanayoingia kwa kasi katika teknolojia hiyo.
Ingawa utajiri wake umepungua, Musk bado anashikilia nafasi ya kwanza kama mtu tajiri zaidi duniani. Hata hivyo, hatima ya Tesla na utajiri wake kwa jumla itategemea hatua atakazochukua ili kurejesha imani ya wawekezaji na wateja.