Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amekumbuka saa za mwisho za maisha ya baba yake, Alhaj Omary Mchengerwa, akisema: “Nitamkumbuka baba kwa ucha Mungu wake na uzalendo wake wa juu.”
Mzee Mchengerwa alifariki alfajiri ya leo, Februari 24, 2025, katika Mji Mtukufu wa Madina, ambapo alikuwa akifanya Ibada ya Umrah kwa muda wa siku 10 katika Makkah na Madina.
Waziri Mchengerwa alithibitisha kifo hicho, akisema: “Amesema kuwa atazikwa leo katika msikiti wa Haram Madina (msikiti wa Mtume saa saba mchana).”
Waziri Mchengerwa, ambaye alikuwa akirejea kutoka ziara ya Rais, alisema baba yake alikuwa amekamilisha ibada yake Makkah na alitarajiwa kurudi nyumbani kesho Jumanne.
Akielezea kifo cha baba yake, Waziri Mchengerwa alisema jana alipata changamoto ya mafua na alilazimika kupumzika. Usiku alishtuka na kutaka kuwahi sala, lakini alielezwa atangojea hadi alfajiri.
Baada ya kupatiwa dawa, hali yake ilionekana kuzorota na kupelekwa hospitali, lakini walipofika alikufa.
Waziri Mchengerwa ambaye ni Mbunge wa Rufiji amesema baba yake alikuwa mtu wa ibada nyingi, mwenye upendo, na mzalendo wa kweli ambaye alifanya kazi katika sekta ya mafuta bila kushiriki katika rushwa wakati wote wa utumishi wake.
Kuhusu elimu yake, Waziri Mchengerwa alieleza kuwa baba yake alikuwa msomi mzuri, akijulikana kwa kutumia Kiingereza katika mawasiliano, hata aliandika ujumbe mfupi kwa wajukuu zake.
Waziri Mchengerwa alihitimisha mazungumzo hayo kwa kusema, “Kifo chake kimekuja kwa namna ya kumfurahisha kila Mwislamu, akifariki kwenye eneo tukufu la Madina, ambapo Mtume Muhammad alizikwa.”
Kwa mujibu wa ratiba ya familia, dua ya kisomo itafanyika kesho Jumanne jimboni Rufiji, Mkoa wa Pwani, na Jumatano itaandaliwa dua nyumbani kwa marehemu Alhaj Omary Mchengerwa Yombo, jijini Dar es Salaam.