Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala kimewaonya wanachama wake kuhusiana na kampeni kabla ya wakati, ikiwa ni tahadhari ya hatua za kinidhamu kwa yeyote atakayebainika kuvunja kanuni hizo.
Katika kikao cha Halmashauri Kuu cha CCM Wilaya kilichofanyika hivi karibuni, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, alieleza wazi kuwa wanachama wanaotukana wenzao na kuanza kampeni kabla ya wakati watachukuliwa hatua stahiki.
Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Sylivester Yared, alisisitiza kuwa mgombea yeyote hatakubalika kupita bila kupingwa. Yared aliongeza kuwa hawataruhusu wanachama kukusanya wajumbe au kugawa fedha katika kipindi hiki amhali akisisitiza juu ya kufuata maelekezo yaliyotolewa na Katibu Mkuu.
“Tumeweka msisitizo kwamba hakuna mtu atakayeweza kuzuia kamati kufanya kazi zao, na tunawataka madiwani, wabunge na wenyeviti wa mitaa kutimiza majukumu yao ipasavyo,” alisema Yared.
Katika taarifa nyingine, CCM Wilaya ya Ilala imeridhika na ripoti ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya, Edward Mpogolo. Taarifa hizo zilionyesha mafanikio katika miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa shule na vituo vya afya.
Pia, chama kimepewa siku saba kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha tanki la maji Bangulo linaanza kufanya kazi ili wananchi wapate huduma ya majisafi.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alitangaza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 317 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu na miundombinu.
Mpogolo alisisitiza jinsi fedha hizo zitakavyosaidia kuboresha huduma kwa wananchi na kuondoa adha zilizokuwepo. Alisema tanki la Bangulo linaendelea kujazwa maji na wanatarajia huduma hiyo kuanza kutolewa hivi karibuni.