ECNETNews, Arusha
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, ametangaza kwamba sheria iliyolazimisha kampuni ya simu ya Vodacom kusajili asilimia 25 ya hisa zake katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) imeleta athari mbaya katika sekta hiyo.
Waziri Silaa alieleza katika kikao kazi na wadau wa sekta ya mawasiliano kwamba, katika uchumi wa soko huria, ni muhimu kutoa nafasi kwa nguvu za soko badala ya kutunga masharti makali.
Akiweka wazi, Silaa alisema kuwa kwa kawaida, makampuni hujisajili katika masoko ya hisa kama njia ya kuongeza mitaji, lakini tofauti na hali hiyo, mwaka 2017 ilitunga sheria iliyowalazimisha makampuni, hususan Vodacom, kujiunga na DSE.
“Katika suala la kujisajili kwenye soko la hisa, kanuni za kibiashara zinahitaji kampuni inayotaka kuongeza mitaji kujiunga. Hata hivyo, mwaka 2017 serikali ilitunga sheria iliyowalazimisha wapange njia ya kujiunga. Nafasi ya Vodacom kwenye soko inatufanya twajiulize, ni lini wengine watajiunga, lakini hali ya wale waliojiunga haijakuwa bora,” alisema Waziri Silaa.
Akiwa akijibu maswali kutoka kwa wadau, Silaa alikiri kwamba serikali ilipokutana na changamoto zinazohusiana na sharti hilo, na kusisitiza kwamba matokeo ya shuruti hizi ni kama yaliyokumba Vodacom tangu mwaka 2017.
“Kama serikali kuanzisha shuruti katika sekta, basi matokeo yake yanaweza kuwa kama haya. Nadhani ni wakati muafaka kwa serikali kurudi kwenye meza ya mazungumzo na wadau kwa ajili ya kutathmini hatua zinazofaa kuchukuliwa,” alisisitiza Silaa.
Aliongeza kuwa kutokana na uzoefu hasi wa Vodacom, kuna uwezekano wa Bunge kukutana na kufanya tathmini ya sheria hiyo ili kukabiliana na matatizo yaliyotokea.
Silaa alijibu swali kuhusu hatua za serikali kusaidia wananchi ambao walishurutishwa kununua hisa za Vodacom mwaka 2017 na bado hawajui hatima ya uwekezaji wao.
Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa serikali kutafakari uamuzi wa awali wa kulazimisha Vodacom kujiunga na soko la hisa kabla ya kuwekwa mazingira rafiki, ambayo yamezalisha hali ya sintofahamu miongoni mwa wawekezaji.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa thamani ya hisa za Vodacom iliporomoka kutoka shilingi 850 mwaka 2017 hadi shilingi 740 mwezi Machi mwaka jana, ikiwa ni kupungua kwa shilingi 110.