Arusha – Serikali imeanzisha kampeni mpya ya kudhibiti vitendo vya utapeli na ulaghai mitandaoni, ambayo inalenga kulinda watu binafsi na taifa kwa ujumla, na hivyo kusaidia katika maendeleo ya nchi.
Kampeni hii, inayoitwa ‘Sitapeliki’, ilizinduliwa leo na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, wakati wa kikao kazi kilichofanyika jijini Arusha. Waziri Slaa alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu mbinu zinazotumiwa na matapeli wa mtandaoni, na kujengea jamii uwezo wa kujikinga dhidi ya ulaghai.
"Kampeni hii inakusudia kutoa maarifa na kuhamasisha jamii kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vitendo vya utapeli mtandaoni," alisema Slaa. Aliendelea kufafanua kwamba, ulaghai unachangia katika kuogopa kwa watumiaji kufanya miamala kupitia mifumo ya kidijitali, na hivyo kuhatarisha juhudi za Serikali katika kutoa huduma za kiuchumi na kijamii.
Waziri Slaa alieleza kuwa, anatumaini kampeni hii itatekelezwa kwa ufanisi ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuleta uelewa juu ya njia za kujikinga. Aliongeza kuwa, kuimarika kwa usalama wa mtandao kutawapa wananchi imani zaidi ya kutumia huduma za kidijitali, na hivyo kuimarisha uchumi wa kidijiti.
Katika kikao kazi hicho, Waziri aliweka wazi mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya mawasiliano, ikiwemo upanuzi wa mtandao wa mkongo wa taifa katika wilaya 109, sawa na asilimia 78. Kufikia Desemba 2024, kadi za simu zilizosajiliwa zinatarajiwa kuwa milioni 86.8, hivyo kuruhusu Serikali kukusanya mapato kutokana na huduma za kidijitali.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mohammed Khamis Abdulla, alieleza kuwa kikao hiki kimejikita katika kutathmini utekelezaji wa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa miaka 10, kuanzia mwaka 2024 hadi 2034, ambao utaanzisha nguzo za kuimarisha miundombinu ya kidijitali, utawala, na mazingira wezeshi.
Wakazi wa Kata ya Sekei, jijini Arusha, wamepongeza juhudi hizi, wakisema kampeni ya ‘Sitapeliki’ itasaidia kupunguza vitendo vya kihalifu mitandaoni na kuimarisha usalama wa watumiaji.