Unguja. Katika kipindi cha Januari mwaka huu, Zanzibar ilikaribisha wageni 84,069, huku wataalamu wa uchumi na takwimu wakitoa mapendekezo ya kuongeza vivutio vya utalii ili kuepusha wageni kuishia tu kwenye hoteli. Wataalamu hao wamesema ni muhimu kuimarisha matangazo ya vivutio hivyo, hasa katika masoko ya China na Afrika, ili kuvutia idadi kubwa zaidi ya wageni.
Shamy Chamicha, mtaalamu wa uchumi na takwimu kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tawi la Zanzibar, alieleza kuwa kuongezeka kwa wageni ni lazima kuendane na uvumbuzi wa vivutio vingi ili kuhakikisha fedha walizokuja nazo zinabaki nchini. “Wageni wanapofika nchini, kuna umuhimu wa kuwapa vivutio vya kutembelea ili kuchangia mzunguko wa uchumi. Iwapo watakaa tu kwenye hoteli, fedha hizo zitarejea walikotoka,” alisema Chamicha.
Estela Ngoma Hassan, mchumi mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza), alisisitiza kuwa wadau wa utalii wana jukumu la kutangaza sekta hiyo katika masoko ya Afrika na China ili kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea Zanzibar.
Hassan Amer Vuai, ofisa kutoka Kamisheni ya Utalii, aliongeza kuwa kamisheni imejipanga kutangaza sekta ya utalii katika mikoa hiyo na India ili kuvutia wageni wengi zaidi.
Fatma Hilali Mohammed, mtakwimu kutoka Kitengo cha Utalii, alionyesha kuwa kuna upungufu wa asilimia 8.2 katika idadi ya wageni ikilinganishwa na 91,611 walioingia Desemba 2024. Kati ya wageni hao, 62,125 (asilimia 73.9) walitoka Bara la Ulaya, wakati Afrika ilichangia wageni 10,390 (asilimia 12.4).
Bara la Amerika lilikuwa la tatu kwa kuingiza wageni 5,546 (asilimia 6.6), na Bara la Oceania kuwa la mwisho kwa wageni 840 (asilimia 1.0) kwa Januari 2025. Italia ilileta wageni 11,725 (asilimia 13.9), ikifuatiwa na Poland walioleta 8,150 (asilimia 9.7), na Ufaransa 7,983 (asilimia 9.5).
Kati ya wageni wote, 75,767 (asilimia 90.1) waliingia kupitia viwanja vya ndege, huku 8,302 (asilimia 9.9) wakifika kupitia bandarini. Kwa mujibu wa mtakwimu huyo, idadi ya wageni walikuwa 40,229 (asilimia 47.9) wakiume na 43,840 (asilimia 52.1) wanawake.
Fatma alibainisha kuwa asilimia 99.5 ya wageni walikuja Zanzibar kwa ajili ya mapumziko, asilimia 0.4 walitembelea ndugu na marafiki, na asilimia 0.1 walikuwa na sababu nyingine kama biashara na mikutano.
Mrakibu wa Uhamiaji, Shariff Bakar Shariff, alieleza kwamba wageni wengi wanaingia Zanzibar sasa wakiwafuata masharti tofauti na miaka iliyopita. Bakar Mussa Yussuf, meneja wa Tehama kutoka Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC), alitaja kwamba wageni wameonyesha utayari wa kuchangia bima ya msafiri, ambayo inawafaidia wanapopatwa na matatizo nchini.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilianzisha bima ya msafiri, ambapo kila mtalii anapaswa kulipa Dola 44 za Marekani, ambayo humsaidia anapougua akiwa nchini. Bima hii imeanza kutumika rasmi Oktoba mosi, 2024.