Dodoma – Bunge la Tanzania limefanya maamuzi makubwa kuhusu ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, likiwemo kufanya tathmini ya kina kuhusu hasara zilizotokana na dosari za awali za usanifu na kuweka uwajibikaji wa gharama kwa pande zinazohusika na mkataba.
Maamuzi haya yalifikiwa leo, Februari 12, 2025, baada ya Naibu Spika, Mussa Zungu, kuwahoji wabunge kuhusu mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Wengi wa wabunge walikubali mapendekezo hayo kwa kutoa majibu ya ‘ndiyo.’
Hatua hii inafuatia taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa PAC, Nagenjwa Kaboyoka, kuhusu ukaguzi wa mradi huo kwa kipindi cha Februari 2024 hadi Januari 2025. Wabunge walikagua na kujadili taarifa hiyo kabla ya kufikia maazimio.
Kaboyoka alisisitiza kwamba ukaguzi wa kiufundi wa ujenzi wa uwanja wa Msalato umezihusisha changamoto kadhaa katika utekelezaji wa mradi. Alitaja dosari zikihusisha uandaaji wa mipango, usanifu wa mradi, usimamizi wa mikataba, manunuzi, na ucheleweshaji wa malipo.
Aliongeza kuwa changamoto hizo zinaathari za kifedha kwa Serikali, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa gharama za ujenzi kwa kiasi cha Sh6.97 bilioni, kutokana na sababu mbalimbali, pamoja na adhabu ya riba ya Sh322.721 milioni kutokana na kucheleweshwa kwa malipo kwa wakandarasi.
Kaboyoka alieleza kuwa kucheleweshwa kwa mchakato wa kupata mkandarasi wa pili wa ujenzi wa miundombinu kunachangia kuongezeka kwa gharama. Alisisitiza kuwa Bunge linaazimia Serikali kufanya mapitio ya vipengele vya mikataba ili kuweka usawa wa malipo kwa gharama zinazoongezeka na kuhakikisha upande uliohusika unawajibika.
Ameshauri Serikali kuhakikisha Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wanasimamia mradi huu kwa makini, huku wakifanya tathmini ya kina kuhusu hasara zilizotokana na dosari za awali za usanifu.
Kaboyoka alifafanua kuwa gharama za ujenzi wa mradi zilikuwa zinakadiriawa kuwa Dola za Marekani 329.47 milioni, ambapo Benki ya Maendeleo ya Afrika ilikubali kutoa mkopo wa Dola za Marekani 271.63 milioni, na Serikali ilitarajiwa kuchangia Dola za Marekani 57.84 milioni.
Ukaguzi huo ulibaini kuwepo kwa wahandisi wasiokuwa wamesajiliwa kufanya kazi katika mradi, huku ujenzi wa majengo ukianza bila ya kuwa na hatimiliki na vibali vya ujenzi, kinyume na kanuni za ujenzi wa mipango miji.
Amesema upembuzi yakinifu ulibaini changamoto kutokana na matumizi ya mbinu zisizo za kitaalamu, ambapo ndege nyuki (drones) zilitumika kupima mwinuko wa ardhi bila kusafisha eneo, na hivyo kuathiri utekelezaji wa mradi kutokana na viwango halisi na michoro.
Wabunge walisisitiza kuwa mabadiliko haya yamesababisha gharama kupanda na kuongezeka kwa malipo yasiyokuwa na msingi. Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Ummy Ndelianga, aliahidi kuwa Serikali itatekeleza maazimio yote yaliyofanywa na kamati.