Musoma. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa kutoka mkoa wa Mara, Christopher Gachuma, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kemirembe Lwota, walihusika katika ajali ya gari jana Februari 9, 2025, wakati wakielekea kumpokea Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira.
Akizungumza leo Februari 10, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, alithibitisha kuwa Lwota na Gachuma walipata majeraha katika ajali hiyo na walikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa matibabu.
Kamanda Lutumo alifafanua kuwa "Katika gari kulikuwa na watu watatu; Christopher Gachuma, Kemirembe Lwota, na dereva, wakiwa wanatokea Mugumu kuelekea Tarime. Wote walikimbizwa Bugando kwa usafiri wa ndege kutoka Fort Ikoma."
Amesema ajali hiyo ilitokana na gari aina ya Toyota Landcruiser V8 kuacha njia na kupinduka, na kusababisha majeraha kwa watatu hao. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, amesema majeruhi wote wanaendelea vizuri, huku akiongeza kuwa Lwota anatarajiwa kusafirishwa usiku huu kwenda Dar es Salaam kwa matibabu zaidi, wakati Gachuma akiruhusiwa.
"DC ataondoka usiku huu kwenda Dar es Salaam kwa matibabu zaidi ingawa kwa sasa hali yake sio mbaya," aliongeza Mtambi.
Wasira alikuwa na ziara katika wilaya sita za mkoa wa Mara, ambapo alifanya vikao na wanachama wa CCM kabla ya kuendelea na ziara yake mkoani Simiyu.
Endelea kufuatilia ECNETNews.