KATIBU Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Dk. Kedmon Mapana, amewataka waandaaji wa matamasha nchini kutilia mkazo juhudi za kusaidia jamii pamoja na burudani.
Dk. Mapana alitoa wito huo, Februari 7, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa Kamati Kuu ya Uendeshaji wa Tuzo za Muziki wa Injili Tanzania (Tanzania Gospel Music Awards – TMGA), akisisitiza kuwa sekta ya sanaa inaendelea kukua kwa kasi.
Katika hotuba yake, Dk. Mapana alisema BASATA inaunga mkono kurejeshwa kwa tuzo hizo, akionyesha matumaini ya kuimarisha thamani ya muziki wa injili nchini.
“Takwimu zinaonyesha kuwa muziki wa injili unaongoza kwa kusikilizwa. Kenya na Marekani ni maeneo yanayothamini muziki huu zaidi. Hongereni kwa kufanikisha kurejea kwa tuzo hizi, kwani zimekuwa zikikosekana kwa muda mrefu,” alisema Dk. Mapana.
Aliendelea kusema kuwa ni muhimu kwa Kamati Kuu ya TMGA kuhakikisha kwamba mchakato wa tuzo hizo unafuata vigezo vilivyowekwa ili kutoa matokeo yanayofanana na matarajio ya jamii.
“Ni wajibu wetu kusimamia taratibu zote ili kuepusha malalamiko au changamoto zinazoweza kuathiri ufanisi wa tuzo hizi,” aliongeza.
Mwenyekiti wa Kamati ya TMGA, Emmanuel Nnko, alisisitiza kuwa tuzo hizo zitakuwa na lengo la kutambua juhudi za wasanii wa muziki wa injili nchini.
“Hatufanyi muziki wa aina moja pekee; tunajitahidi kugusa vipengele mbalimbali ili kuhakikisha kila msanii wa injili anapata nafasi ya kushiriki. Lengo letu ni kukuza muziki wa injili na kutambua juhudi za wasanii katika uandaaji wa nyimbo za ubora,” alisema Nnko.
Alifafanua kuwa kamati itatumia mfumo maalum wa kidigitali kupokea kazi za wasanii, hivyo kurahisisha usimamizi wa uteuzi na kuhakikisha uwazi katika mchakato huo.
“Wasanii watatuma kazi zao kupitia mfumo maalumu, na tutashirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha tuzo hizi zinafanyika kwa viwango vya kimataifa,” aliongeza.