CHAMA cha Wamiliki wa Malori Wadogo na Wakati Tanzania (TAMSTOA) kimeiomba Serikali kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wahusika wa sekta ya usafiri, hususan kamatakamata ya magari na ufinyu wa barabara.
Katika Mkutano wa Tano wa mwaka 2024 uliofanyika Februari 5, 2025, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TAMSTOA, Shaban Chuki, alisema kwamba changamoto nyingi zinakabili sekta hiyo, ikiwemo ushuru wanaotozwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
Mwenyekiti huyo aliwasilisha ombi kwa Serikali kwa niaba ya wanachama wenzake, akitaka kuondolewa kwa vikwazo vya usafiri na kujengewa barabara katika maeneo yenye barabara nyembamba na ambayo malori mengi hupita.
Akizungumza kuhusu barabara inayotoka bandarini kuelekea Morogoro, Chuki alionya kwamba barabara hiyo ni finyu na inahitaji kuimarishwa ili kukabiliana na ongezeko la magari, huku akisema kwamba miundombinu katika baadhi ya maeneo bado inahitaji uboreshaji mkubwa.
Amesema kuwa Wilaya za Temeke na Ubungo ndizo zinazoathirika zaidi kutokana na ukamataji wa malori licha ya kwamba tatizo hilo linatokana na ukosefu wa maeneo sahihi ya kupaki.
TAMSTOA pia imeomba kuangaliwa kwa utaratibu wa utozwaji wa ushuru katika eneo la Mikumi, Morogoro, kwani umekuwa ukisababisha madhara makubwa kwa wamiliki wa malori.
“Magari yote yanayobeba mizigo kutoka nje ya nchi yanategemea bandari ya Dar es Salaam, na hivyo ni muhimu kwa viongozi wa Temeke kutambua kuwa ongezeko la malori ni fursa na sio kero,” alisema Chuki.
Amesema kamatakamata bila utaratibu imekuwa changamoto muhimu, ikichangia katika ongezeko la uhalifu na kukosekana kwa usalama kwa madereva.
TAMSTOA imelazimika kuiomba Serikali kutafuta maeneo maalumu ya kupaki malori na kuitaka TRA kukabiliana na matatizo yanayoibuka katika eneo la Mikumi, Morogoro, ambapo ripoti za rushwa zimeibuka.
Chuki alieleza kuwa licha ya juhudi za mwaka 2024 katika kupunguza matatizo ya kamatakamata malori hasa katika wilaya za Temeke na Ubungo, bado kuna changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa haraka kutoka kwa Serikali.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya chama, alifafanua kuwa TAMSTOA sasa ina wanachama wapatao 900 wanaomiliki zaidi ya malori 26,000, ambayo yameweza kutoa ajira kwa watanzania 52,000.
Chuki alisema kuwa TAMSTOA inajitahidi kuimarisha ushirikiano na Serikali katika kutetea maslahi ya wanachama na kuhakikisha mazingira bora ya biashara ya usafirishaji yanakuwepo ili kuongeza pato la Taifa.
Kwa mujibu wa takwimu, malori hayo yanatumia zaidi ya lita milioni 62.4 za mafuta kwa siku, ikiwa ni gharama ya zaidi ya shilingi milioni 187 kwa mwaka, huku sekta ya usafiri ikichangia kubwa katika pato la Taifa.
Kuhusu suala la madereva wa Tanzania walioathirika katika mji wa Goma, Chuki alishukuru hatua za Serikali katika kuwaokoa.
Geoffrey Silanda, mwakilishi wa Serikali katika mkutano huo, alieleza kuwa TAMSTOA imekuwa ikishirikiana na Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya usafiri, hususan upimaji wa mizigo na ukamataji katika maeneo yaliyo na changamoto.
Mkutano huo pia ulikuwa na lengo la kufanya tathmini ya miaka 10 tangu chama kilipoanzishwa mwaka 2014, na kaulimbiu ilikuwa ni “Kulinda na kutetea maslahi ya wanachama, ubunifu na kuinua wamiliki wa malori wadogo na wa kati hadi viwango vikubwa. Kushirikiana na Serikali kutatua changamoto za sekta ya usafirishaji.”