Dar es Salaam. Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani umethibitisha kuwa kuna watu 24 wanaoshikiliwa na Mamlaka ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani (ICE) kwa kuishi nchini humo kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa taarifa za ubalozi, watu wanne tayari wameshakamilisha taratibu za kimahakama na hivyo wanatarajiwa kurejeshwa Tanzania muda wowote kuanzia sasa, wakati watu 20 waliobaki wako kwenye hatua mbalimbali za kesi zao za uhamiaji.
Ubalozi huo umesema kuwa bado hawajapokea taarifa ya tarehe mahsusi ya kurejeshwa kwa Watanzania hao. Hata hivyo, tayari umeombwa nyaraka za kusafiria za Watanzania wawili kati ya wanne walioamriwa kuondolewa nchini Marekani, na hivyo inatarajiwa kuwa watasafirishwa karibuni.
Hatua hii inatokana na mkakati wa Rais wa Marekani wa kuondoa wahamiaji wote wanaoishi nchini humo bila vibali. Taarifa ya ICE ilieleza kuwa hadi Novemba 24, 2024, wahamiaji 1,445,549 waliorodheshwa kwa ajili ya kurejeshwa nyumbani.
Kati ya wahamiaji hao, Tanzania ina idadi ya watu 301, ikiwa nyuma ya Kenya, Burundi, Uganda, na Rwanda. Katika majibu yake kwa maswali yaliyowasilishwa hivi karibuni, ubalozi ulimhakikishia Mwananchi kuwa Watanzania watakaorejeshwa wataruhusiwa kusafiri kwenda nchi nyingine bila kizuizi, ingawa kwa upande wa Marekani, wanaweza kuomba viza baada ya miaka 10.
Watanzania watakaorejeshwa watanukuliwa na Idara ya Uhamiaji mara watakapofika nyumbani, na wataweza kuendelea na maisha yao kama raia wengine wa Tanzania.
Ubalozi umesisitiza mfumo wa ushirikiano na mamlaka za uhamiaji wa Marekani ili kuthibitisha uraia wa waliowekwa vizuizini na kutoa nyaraka za kusafiria kwa wahusika. Kutokuwa na vibali maalumu ni kosa la kisheria katika nchi yoyote.
Mkurugenzi wa Diaspora Tanzania, Kelvin Nyamori, amewaonya watu kuhusu changamoto watakazokumbana nazo ikiwa watajifanya kuwa wakimbizi bila sababu halali. Alisema, “Kuna sheria za uhamiaji za kila nchi, na ni muhimu kufuata taratibu na kuwa na vibali wanapokuwa wakitoka nje ya nchi.”