KLABU ya mchezo wa kriketi nchini, Aga Khan SC, imeingia mkataba wa miaka miwili na kampuni ya HÄFELE East Africa Limited, ikitekeleza udhamini wa jezi za msimu wa 2025/2026.
Mkataba huu uliosainiwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam, unaleta matumaini makubwa kwa klabu katika juhudi zake za kukuza mchezo wa kriketi nchini. Uongozi wa klabu umesema udhamini huu utasaidia sana katika maendeleo ya mchezo.
Taarifa kutoka uongozi wa klabu inasema, “Mkataba huu unathibitisha dhamira ya kampuni ya HÄFELE kuzalisha bidhaa bora na kujitahidi kuendeleza vipaji vya mchezo wa kriketi nchini.”
Kiongozi Mwandamizi wa klabu hiyo, Ayzaz Jassani, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huu, akisema, “Ushirikiano huu utakuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya klabu na utaimarisha taswira ya taasisi hizo mbili katika ulimwengu wa michezo.”
Amesema, “Kila mchezaji wa Aga Khan SC atavaa jezi hii kwa heshima, akiwakilisha maadili ya ubora na utendaji,” aliongeza.
Mchezaji mwandamizi, Vipin Abraham, alieleza kwamba udhamini huu unatoa fursa ya kuinua mchezo na kuimarisha mazingira ya wachezaji chipukizi, ambao ni lengo kuu la klabu.
Mkurugenzi Mtendaji wa HÄFELE East Africa Limited, Snehal Bakrania, alisisitiza umuhimu wa ubora katika mkataba huu. “Tunaona dhamira ya kuimarisha viwango kati ya kampuni yetu na mchezo wa kriketi. Katika mchezo, wachezaji wanajitahidi kuboresha mbinu zao kama ambavyo HÄFELE inaendelea kuwa mbunifu ili kuboresha huduma zetu,” alisema Bakrania. “Leo tunasherehekea historia ya klabu, tukionyesha ushirikiano, usahihi, na ubunifu.”