Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA Amos Makalla, ametoa taarifa kuhusu Soko la kisasa la Chuwini, akisisitiza kwamba litaleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa Zanzibar.
Amesema hayo leo, Ijumaa, Januari 31, 2025, alipokuwa akikagua mradi huo wa kimkakati wakati wa ziara yake ya mikoa sita ya kichama visiwani Zanzibar.
Soko hili litakuwa kubwa zaidi ya soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, likitarajiwa kuhudumia wafanyabiashara zaidi ya 4,000 kwa wakati mmoja, tofauti na Kariakoo ambayo inaweza kuchukua wafanyabiashara kati ya 3,000 hadi 3,500.
Pia, Makalla amepongeza ubunifu wa kuchanganya soko pamoja na kituo cha mabasi, akibainisha kuwa hatua hii itachangia pakubwa katika ukuaji wa biashara.
Alisisitiza umuhimu wa kushirikiana kati ya viongozi, akiwapongeza Dk. Samia na Dk. Hussein Mwinyi kwa jitihada zao katika kuleta maendeleo. “Nimejionea kwa macho yangu maendeleo ya soko hili na ni dhahiri kwamba waliyoyafanya ni ya kihistoria,” alisema Makalla.
Aliongeza kuwa, “Wale wajasiriamali kutoka maeneo mbalimbali wanapaswa kufika na kushuhudia kazi kubwa iliyo tekelezwa, kwani kuona ni kuamini,”