Njombe. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, mkoani Njombe, wamependekeza kupunguzwa kwa bei ya ushuru wa mazao ili kudhibiti utoroshaji wa mazao unaofanywa na wafanyabiashara wadanganyifu, hatua ambayo inatarajiwa kusaidia kuzuia hasara kwa halmashauri.
Pendekezo hilo lilitolewa katika baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe lililofanyika leo, Februari Mosi, 2025. Madiwani wameeleza kuwa kiwango cha ushuru wa mazao katika halmashauri hiyo ni cha juu ukilinganisha na halmashauri nyingine katika mkoa, hali inayochangia wafanyabiashara kutorosha mazao na kupata vibali katika halmashauri zisizokuwa na ushuru mzito.
Diwani wa Itulahumba, Thobias Nkane, alifafanua kuwa ushuru wa mahindi kwa gunia la kilo 100 unafikia Sh1,500, wakati ambapo halmashauri nyingine hutoza Sh1,000. Hali hii inawafanya wafanyabiashara kuhamasika kuhamia maeneo mengine kwenye biashara zao.
"Ushuru wa mahindi unawafanya wafanyabiashara kuhamia halmashauri zingine," alisema Nkane.
Diwani wa Mdandu, Annaupendo Gombela, aliongeza kuwa ushuru wa Sh1,500 kwa gunia unawapata wakulima katika mazingira magumu, hususan kwa kukosa soko la uhakika.
"Kwa kupunguza bei hii, kutasaidia kuvutia wanunuzi wengi wa mazao kuja kwenye halmashauri na wakulima wataweza kupata kipato," alisema Gombela.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Onesmo Lyandala, alisema kuwa katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025, halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya Sh3.1 bilioni kutoka vyanzo vya ndani. Lyandala alisisitiza kuwa tayari kuna pendekezo la kupunguza ushuru wa mahindi kutoka Sh1,500 hadi Sh1,000 ili kuvutia wanunuzi na kuongeza mapato ya halmashauri hiyo.