Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amethibitisha kuwa maandalizi ya Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika, unaokusudia kuharakisha upatikanaji wa umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030 (Mission 300), yamefikia asilimia 95. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika tarehe 27 na 28 Januari katika jiji la Dar es Salaam.
Dkt. Biteko alitoa taarifa hiyo Januari 15, 2025, baada ya kufanya ukaguzi wa maandalizi ya mkutano katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) akiwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Amesema Wakuu wa Nchi 54 kutoka Bara la Afrika wanatazamiwa kushiriki, pamoja na viongozi wa Mawaziri wa Fedha na Nishati, Marais wa Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika, na viongozi kutoka Jumuiya ya Ulaya na Umoja wa Afrika. Maandalizi ya ukarabati wa ukumbi wa JNICC yanaendelea ili kuhakikisha mkutano unafanikiwa.
“Vilevile, kazi zinaendelea katika usajili na uthibitisho wa wageni watakaoshiriki, na ukarabati wa maeneo mengine yatakayotumika kwenye mkutano huu, ni wajibu kuwapongeza viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa hatua zilizofikiwa,” alisisitiza Dk. Biteko.
Mkutano wa M300 umekuwa kivutio kwa Wakuu wa Taasisi nyingi za Kimataifa, na uchaguzi wa Tanzania kuwa mwenyeji unatokana na Diplomasia bora ya Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambayo imeimarisha uhusiano wa Tanzania kimataifa.
Aliweka wazi kuwa mafanikio katika sekta ya Nishati nchini, kama vile usambazaji wa umeme vijijini, ni moja ya sababu za Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji. Kuwepo umeme katika vijiji vyote 12,318 na Vitongoji 34,000 kati ya 64,274 ni dalili ya maendeleo makubwa.
Dkt. Biteko alisisitiza kuwa mkutano utaweza kuongeza idadi ya Watanzania watakaounganishwa na umeme ifikapo mwaka 2030 hadi milioni 13.5 kutoka milioni 5.2 iliyopo sasa, na kupelekea kusainiwa kwa mikakati ya usambazaji umeme kwa wananchi chini ya mwavuli wa WB na AfDB.
Faida nyingine za mkutano wa M300 ni pamoja na kuongezeka kwa fursa za uwekezaji, kuimarisha biashara, na kuongeza heshima ya Tanzania katika nyanja za kimataifa. Dk. Biteko amewataka Watanzania kuupokea mkutano huo kwa mikono miwili, huku akihimiza amani na utulivu kabla ya mkutano huo wa kihistoria.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameongeza kuwa maandalizi ya kupokea ugeni huo yako katika hatua za mwisho, na baadhi ya mitaa itafungwa ili kuruhusu maonesho na utalii wa ndani, ikiwa ni sehemu ya kuelekea kwenye mkutano huo.