Seoul. Uchunguzi umebaini kwamba vifaa vya kurekodi taarifa ya mwenendo wa ndege ya Shirika la Jeju nchini Korea Kusini, viliacha kufanya kazi dakika nne kabla ya ndege hiyo kupata ajali na kulipuka.
Ndege hiyo aina ya Boeing 737-800, ikiwa na abiria 181 wakiwemo 175 wa kawaida na wahudumu sita, ilipata ajali ambapo watu 179 walifariki, wahudumu wawili wakiweza kupona.
Ajali hii ilitokea Desemba 29, 2024, ambapo ndege hiyo ilikabiliwa na hitilafu katika mfumo wa gia ya kutua, na ikashindwa kutua ipasavyo kwa kutumia sehemu ya tumbo (uvungu) wa ndege hiyo, kabla ya kugonga nguzo zilizokuwa zimejengwa mwishoni mwa njia ya kurukia.
Uchunguzi unaonyesha kwamba ajali hii inachukuliwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini Korea Kusini katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, huku maofisa wakitumai kwamba vitu vya kurekodi taarifa vya ndege, maarufu kama sanduku la kurekodi (Flight Data Recorder – FDR) na kifaa cha kurekodi sauti za wahudumu na marubani (Cockpit Voice Recorder – CVR), vilikoma kufanya kazi kabla ya ajali hiyo.
Wizara ya Usafirishaji ya Korea Kusini imetoa taarifa kuwa kufanya kazi kwa vifaa hivyo kumeshindwa kabla ya tukio hilo, na kwamba uchunguzi unatarajiwa kufanyika ili kubaini sababu za tatizo hili.
Katika taarifa hiyo, wizara ilisisitiza umuhimu wa uchambuzi wa tarifa hizo katika kuchunguza ajali ya ndege, na ilisema kuwa kifaa cha CVR kimepelekwa Marekani kwa uchunguzi zaidi. Kifaa cha FDR pia kimeharibiwa vibaya na kimepelekwa kwa uchunguzi baada ya kushindwa kuchota taarifa nchini Korea Kusini.
Ajali hii ni ya kwanza kusababisha madhara makubwa kwa abiria tangu mwaka 1997. Hadi sasa, sababu halisi ya ajali haijajulikana na uchunguzi unatarajiwa kuchukua muda kabla ya matokeo ya mwisho kupatikana. Video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii inaonesha ndege hiyo ikishindwa kuchomoa gia zote za kutua kabla ya kugonga nguzo.
Rubani alisikika akitoa taarifa ya dharura akieleza kwamba ndege hiyo imegongwa na ndege pori, huku akijaribu kutua kwa dharura. Jeshi la Polisi nchini Korea Kusini lilichukua hatua kwa kuvamia ofisi za Shirika la Jeju, zikitekeleza uchunguzi kubaini chanzo na hatari zinazoweza kutokea kutokana na uzembe wowote utakaoonekana.