Bratislava, Slovakia – Waziri Mkuu Robert Fico ameitaka serikali yake kuzingatia kusitisha misaada ya kifedha na kibinadamu kwa Ukraine, kufuatia uamuzi wa nchi hiyo kugomea ufufuaji wa mkataba wa bomba la usafirishaji wa gesi asilia kutoka Russia.
Fico alitoa kauli hiyo baada ya mazungumzo na Kamishna wa Nishati wa Umoja wa Ulaya, akisema kwamba hatua ya Ukraine inahujumu Slovakia, nchi ambayo inategemea gesi nafuu kutoka Russia.
" hakuna sheria za kimataifa zinazoweza kuzuia usafirishaji wa gesi kupitia Ukraine," alisisitiza Fico kwenye mkutano wa viongozi wa Ulaya huko Brussels.
Slovakia inategemea gesi ya Russia kwa asilimia 60 ya matumizi yake, na Fico alionya kwamba nchi yake inaweza kupoteza dola milioni 515 kutokana na gharama za usafirishaji kutoka vyanzo vingine, wakati hasara ya jumla inaweza kufikia dola bilioni 1.
"Endapo tatizo hili halitatatuliwa, Serikali ya Slovakia itachukua hatua madhubuti kukabiliana na Ukraine," alisema Fico, akionyesha hatua za kutafuta kura ya Veto katika Umoja wa Ulaya ili kuondoa misaada yote kwa Ukraine.
Vilevile, alitishia kurejesha raia wa Ukraine walioko nchini Slovakia na kuikatia umeme Ukraine.
Kauli ya Fico inakuja baada ya ziara yake nchini Russia, ambapo alizungumza na Rais Vladimir Putin, ambaye alihakikishia msaada wa gesi. Kikao kilichokuwa kipango cha kujadili hali hiyo kiliahirishwa baada ya Ukraine kusema haitoshiriki.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Slovakia, Matus Sutaj Estok, alikosoa msimamo wa Ukraine, akisema kuwa umeshindwa kuonyesha mshikamano na mataifa mengine ambayo yanategemea gesi kutoka Russia.
Hadi sasa, Ukraine haijatoa majibu kuhusiana na kauli ya Fico. Slovakia ilipotoa tishio la kukata umeme kwenda Ukraine, Waziri wa Nishati wa Ukraine alisema hakuwa na wasiwasi kuhusu utekelezaji wa tishio hilo.
Kwa upande mwingine, Ukraine inaamini kuwa itaendelea kupokea msaada wa kijeshi na kifedha kutoka mataifa ya Ulaya, huku Rais Zelenskyy akisema kuwa msaada wa kijeshi umezidishwa.