Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC) limewataka watoa huduma kuzingatia matakwa ya leseni zao, kuhakikisha kwamba huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vya madaraja yaliyochaguliwa na abiria.
Katika mkutano uliofanyika leo, Katibu Mtendaji wa LATRA CCC, Daudi Daudi, alieleza kuwa kipindi cha mapumziko ya mwisho wa mwaka kimeongeza mahitaji ya usafiri, mara nyingi kupelekea watoa huduma kufikia nguvu zao za kawaida.
Daudi alisisitiza umuhimu wa abiria kutoa taarifa sahihi pindi wanapokutana na huduma zisizokidhi viwango vinavyolingana na tiketi zao.
“Mara nyingi, mapumziko ya mwisho wa mwaka yanahusishwa na ongezeko kubwa la wasafiri wakielekea maeneo mbalimbali nchini. Hii inamaanisha kwamba watoa huduma wanapaswa kuwa tayari kukabiliana na abiria wengi wapya ambao sio wa kawaida,” alisema Daudi.
Aidha, alikumbusha abiria wajitayarishe mapema kwa ajili ya vyombo vya usafiri wanavyotegemea na kukata tiketi kupitia njia rasmi ili kuepuka usumbufu wa wapigadebe au gharama zisizo rasmi.
Baraza limewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali na kuhakisha usalama wa abiria.