Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linamshikilia dereva wa lori la mafuta, Jackson Kashebo (45), na utingo wake, William Sichone (34), wakituhumiwa kusafirisha vipodozi vyenye viambata vya sumu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa polisi, walikamatwa wakiwa kwenye lori lenye namba za usajili T 747 DDE na tela namba T 330 CJX aina ya Faw. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga, amesema wanatuhumiwa kwa kukamatwa na maboksi 201 ya vipodozi hivyo mnamo Desemba 28, 2024, saa 11:15 asubuhi katika Mtaa wa Keseria, Kata ya Chapwa, wilayani Momba.
Kamanda Senga alifafanua kuwa walikamatwa baada ya polisi kupata taarifa za siri na kuweka mtego ambao ulisaidia kuwatia mbaroni. Wakiwa wamepakia shehena ya vipodozi kwenye vyumba vya kubebea petroli na dizeli wakitokea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), walikamatwa na vipodozi kama vile Extra Clair, Betasol Tube, Pawpaw Cream, Snail White, na bidhaa nyingine mbalimbali.
Katika tukio lingine, polisi kwa ushirikiano na wataalamu kutoka TFRA na Halmashauri ya Mji wa Tunduma, wamewakamata watuhumiwa Gosso Mussa (32) na Prisca Shembe (37), wakazi wa Sogea, Tunduma. Watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa ya kusafirisha mbolea kinyume cha sheria na bila kibali, wakiwa na mifuko 125 iliyofungashwa.
Wanadaiwa walifanya udanganyifu kwa kuuza mbolea ya DAAP Plus ya kampuni ya Minjingu iliyofungashwa kwenye mifuko ya DAP ya kampuni ya Falcon ETG. Wamekamatwa leo Desemba 28, 2024, saa 2:00 asubuhi katika Mtaa wa Unyamwanga, Kata ya Tunduma, wilayani Momba.
Taarifa ya polisi inasema mifuko hiyo ilifichwa kwenye ghala la kuhifadhia bidhaa mbalimbali za pembejeo kwa lengo la kuuza. Kamanda Senga amesema upelelezi wa shauri hili unaendelea na kwamba watuhumiwa wote wanne watafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika.