Dar es Salaam – Mabehewa 264 ya mizigo, yaliyotengenezwa nchini China kwa ajili ya reli ya kisasa (SGR), yamewasili katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), mabehewa hayo yaliwasili nchini jana, Desemba 24, 2024. TRC ilieleza kwamba meli iliyobeba mabehewa hayo iliondoka katika bandari nchini China tarehe Novemba 12, 2024.
Katika taarifa iliyotolewa leo, Desemba 25, 2024, TRC imethibitisha kuwa kati ya mabehewa hayo, 200 yatatumika kubeba makasha (makontena), na 64 yatabeba mizigo isiyofungwa.
Fredy Mwanjala, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa TRC, alisema mchakato wa kuyashusha mabehewa hayo utafuatiwa na majaribio ya awali yatakayojumuisha kuyatembeza mabehewa hayo katika reli yakiwa tupu na yaliyojaa mizigo. "Mabehewa hayo yatakuwa yanatembea kwa kasi ya kilomita 120 kwa saa na, ifikapo wakati wa majaribio, watalaamu wa TRC watahakiki iwapo yamekidhi viwango vilivyowekwa," alisema Mwanjala.
Mabehewa 264 ni sehemu ya jumla ya 1,430 ambayo yanatengenezwa na Kampuni ya CRRC ya China, ikielezwa kuwa TRC ilianza huduma za SGR kati ya Dar es Salaam na Morogoro mnamo Juni 14 mwaka huu, na safari za Dodoma zilianza Julai 25.
Akizindua huduma za abiria za SGR Agosti 1, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza kuwa kuanzishwa kwa treni ya umeme kutaathiri usafiri wa barabara nchini.
"Ingawa tumeona kupungua kwa idadi ya mabasi, ni jambo zuri kwa sababu litapunguza ajali za barabarani," alisema Rais Samia, akiongeza kwamba malori bado yatabaki kuwa muhimu katika maeneo ambayo hayajafikiwa na treni hiyo.
Wachumi, wafanyabiashara, na wamiliki wa malori wamesema kuanza kwa usafirishaji wa mizigo kupitia SGR kutarahisisha biashara na kupunguza gharama za bidhaa. Aidha, uwezo wa treni ya SGR wa kubeba tani 10,000 za mzigo kwa mkupuo umeelezwa kuwa sawa na uwezo wa malori 500.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Augustine Vuma, ameahidi kuwa usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli utaanza rasmi Januari au Februari 2025, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uchumi kupitia sekta ya usafirishaji.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori nchini, Chuki Shaban, sekta yao inabaki kuwa na umuhimu mkubwa licha ya kuanzishwa kwa huduma hizo za reli, na wataendelea kufanya kazi kwa pamoja katika uchumi wa nchi.