Dar es Salaam. Wito wa kutangaza amani katika ngazi ya familia, taifa, na binafsi umeanzishwa ili kuenzi kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Kristo.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Stephano Musomba, amesisitiza kuwa amani ni chachu ya upatanishi miongoni mwa watu. Amesema hayo leo, Jumapili, Desemba 24, 2024, alipohubiri katika ibada ya mkesha wa Krismasi katika Kanisa la St. Peter, Dar es Salaam.
Ameongeza kwamba ni bora kutangaza amani badala ya kuhubiri ugomvi na chuki. “Palipo na amani, pana upendo na ushirikiano, na hivyo panakuwa na upatanisho na uvumilivu baina yetu,” amesema.
Akiendelea na mahubiri yake, Askofu Musomba amebainisha kuwa kutangaza amani ni njia mojawapo ya kuenzi kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Kristo. Amesema kuzaliwa kwa Kristo kunapaswa kuwa fursa ya kuwatafakarisha watu kuhusu wakati walio nao sasa.
“Kila mmoja anapaswa kujiuliza angalau anapoadhimisha Noel, yuko wapi?,” amesema. Ameitaka jamii kuangalia maisha yao ya sasa na kuona kama yanaakisi unyenyekevu alionao Kristo.
“Je, utaweza kukiri kwamba una makosa au umemkosea mwenzako na unaomba msamaha?” amehoji.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa waumini kutangaza habari njema kwa wengine na kuendeleza amani, msamaha, na uvumilivu kwa wakati wote.