Rombo. Serikali imeanzisha usajili wa mwongozo wa watoto wenye ulemavu, ikilenga kutoa fursa kwa watoto wenye changamoto kufundishwa wakiwa nyumbani.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, wakati wa kukabidhi viti mwendo kwa watoto wenye mahitaji maalumu katika wilaya hiyo.
Amesema kwamba Serikali haitamwacha mzazi abebe jukumu la mtoto mwenye ulemavu peke yake, na kwamba ni muhimu kuondoa mtazamo wa kuwaficha watoto wenye changamoto hizo nyumbani.
Profesa Mkenda amewataka maofisa ustawi wa jamii katika maeneo mbalimbali kutoa taarifa za watoto wenye changamoto kubwa ili waweze kusaidiwa kwa njia bora.
“Kwa watoto wenye changamoto kubwa ambao wazazi wao wanakataa kutowaacha wakiwa nyumbani, Serikali itawahudumia kwa kuwapelekea mwalimu nyumbani, hii ni katika kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuimarisha elimu nchini,” alisema Profesa Mkenda.
Amesisitiza kwamba mpango wa Serikali unalenga kuhakikisha kwamba kila mtoto anapata elimu, huku akitaja uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya elimu.
Pia, amesema ni marufuku kwa mwanafunzi yeyote kurudishwa nyumbani kwa sababu mzazi hajatoa mchango wa shule.
Aidha, Profesa Mkenda alimanisha kuwa Serikali tayari imeanza kuchapisha vitabu maalumu kwa watoto wenye mahitaji, hasa wale ambao hawawezi kusoma kwa macho, wakitumia vidole kwa ajili ya kujifunza.
“Kwa mara ya kwanza, vitabu vyote vinavyochapishwa sasa vina maandiko yaliyokuzwa na vile vya nukta nundu, ili kuwasaidia watoto wenye ulemavu wa kuona,” aliongeza.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Raymond Mwangwala, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia haki za watoto wenye mahitaji maalumu na kuwataka wazazi kuacha kuwaficha watoto hawa.
“Sitarajii kuona mzazi akimficha mtoto ndani, hawa ni ndugu zetu, wana haki sawa na watoto wengine, na hawatakiwi kutofautishwa,” alisema.