Dar es Salaam. Matokeo ya uchaguzi wa ndani wa Chama cha Wananchi (CUF) yatatolewa leo, yakisubiriwa kwa hamu ili kubaini hatma ya uongozi wa Profesa Ibrahim Lipumba katika nafasi ya uenyekiti wa chama hicho.
Profesa Lipumba, anayeshiriki uchaguzi huo, anashindana na makada wengine wanane, ikiwa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CUF bara, Maftah Nachuma.
Wagombea wengine ni Ali Hamisi, Athumani Kanali, Juma Nkumbi, Nkunyuntila Chiwale, Wilfred Rwakatare (Mbunge mstaafu wa Bukoba Mjini), na Chifu Yemba (aliyewahi kuwania urais kwa tiketi ya ADC mwaka 2020).
Kumekuwa na hamu kubwa kujua kama Profesa Lipumba atabaki katika nafasi hiyo aliyoshika kwa miaka 25 tangu mwaka 1999, au kama utakuwa mwisho wa enzi yake kama mwenyekiti.
Hali ya ukumbini kabla ya uchaguzi
Mkutano wa uchaguzi umetanguliwa na mkutano mkuu wa kawaida wa chama hicho, ambapo viongozi mbalimbali wa kitaifa walitoa hotuba. Mkutano huu pia ulihudhuriwa na viongozi kutoka vyama vingine vya siasa.
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Benson Kigaila, walishiriki katika mkutano huo. CCM iliwakilishwa na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdalla Hamid.
Kwa upande wa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Naibu Msajili, Sisty Nyahoza, alikuwa miongoni mwa wageni waliokuwepo.
Kamati ya Uchaguzi ilianza kazi yake rasmi saa 5:32, ikiongozwa na Mwenyekiti Mashaka Ngole, ambaye alijitambulisha pamoja na wajumbe wake.
Kukubali na kuingiza wajumbe halali wa mkutano ndani ya ukumbi kulifanyika kabla ya kuchaguliwa mwenyekiti wa muda atakayesimamia shughuli za uchaguzi hadi kutangazwa kwa mwenyekiti mpya.
Wakati wa tukio hilo, wapiga debe kinyemela walionekana wakifanya kampeni kwa wagombea, huku baadhi ya maofisa wa chama wakihusishwa na kampeni ya kumshawishi Profesa Lipumba aendelee kushikilia kiti hicho.
Hadi saa 6:19, uhakiki wa wajumbe halali haujakamilika, na CUF imethibitisha kuwa chaguzi zote za viongozi zitafanyika leo, huku mkutano wa kesho ukitarajiwa kujikita katika hotuba za viongozi pekee.