Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, wanawake zaidi ya 400 kutoka taasisi za serikali na sekta binafsi walitembelea Hifadhi ya Ngorongoro, huku wakishuhudia vivutio mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanyama wakubwa maarufu kama “Big Five”.
Kamishina Msaidizi Mwandamizi anayesimamia idara ya huduma za Utalii na Masoko, Mariam Kobelo, alisema kwamba ujio wa wanawake hao utachangia katika kuhamasisha utalii wa ndani katika hifadhi hiyo. “Tukiwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, tumejikita kutangaza vivutio vya utalii ndani ya eneo hili. Leo tumepokea wanawake karibu 400 kwa kushirikiana na kampuni ya utalii,” alisema Mariam.
Akiendelea, Mariam alisisitiza kuwa NCAA imejipanga vizuri kuhakikisha ziara hii inachochea wengine kutembelea vivutio mbalimbali nchini, sambamba na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kukuza utalii nchini.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa kampuni ya kitalii alisema kwamba kampuni yake imejikita kwenye utalii wa ndani na inaboresha ziara za kutembelea hifadhi mbalimbali. “Kreta ya Ngorongoro ni kivutio kikuu ambacho kimevutia watalii wengi, na leo tumekuja na wanawake karibu 400 kusherehekea Siku ya Wanawake,” alisema.
Bi. Gloria Mziray kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) alieleza kwamba safari yao ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ya kipekee na walifurahia kuona wanyama wakiwa kwenye mazingira yao ya asili.
Bi. Fatuma Abduli kutoka benki ya CRDB alitoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio mbalimbali vilivyomo nchini, huku akisisitiza upekee wa Hifadhi ya Ngorongoro.
Wanawake hao pamoja na watalii wengine wameshuhudia vivutio kadhaa ikiwemo “Big Five”; Faru, Tembo, Chui, Nyati, na Simba. Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kinatarajiwa kufanyika Machi 08, 2025, mkoani Arusha, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, atakuwa mgeni rasmi.